Mahakama ya rufaa nchini Kenya imetoa uamuzi kwa shule za Kikristo kuwaruhusu wanafunzi wa kike wa kiislamu kuvaa Hijabu kama sare za shule.
Shule zinazoendeshwa na Makanisa zilikuwa zimepiga marufuku wanafunzi wa kike kuvaa Hijabu.
Uamuzi huo wa uliotolewa na majaji watatu umekuja baada ya kanisa la kimethodist kupinga muongozo kutoka kwa mamlaka za nchi hiyo kuwaruhusu wasichana wa shule wa Kiislamu kuvaa hijabu au vitambaa vya kichwa katika shule yake.
Wanafunzi wa Kiislamu katika shule ya sekondari ya St Paul Kiwanjani School Kaunti ya Isiolo walipigwa marufuku kuvaa Hijabu na suruali nyeupe pamoja na sare ya shule.
Kanisa hilo lilidai kuwa, uamuzi wa kuwaruhusu wanafunzi wasichana wa Kiislamu kuvaa mavazi tofauti umesababisha uhasama miongoni mwa wanafunzi wa shule hiyo.
Awali Mahakama ya juu nchini Kenya iliunga mkono msimamo wa kanisa na kusema kuwa wasichana hawawezi kuvaa hijabu wakiwa shuleni.
Majaji wa Mahakama ya Kenya wamepinga suala la marufuku ya vazi la hijab nchini na kuunga mkono uhuru wa dini kwa wananchi wote. Shule za serikali zimeruhusu wanafunzi kuvaa Hijabu.
Majaji hao pia wamemhimiza Waziri wa elimu kushauriana na viongozi wa taasisi za taaluma ili kuhakikisha uhuru na haki ya dini haikiukwi wala ubaguzi kutokea.
Jopo la majaji lililoongozwa na mwanasheria Phillip Waki wa mahakama kuu ya rufaa, lilifutilia mbali pendekezo la kuweka marufuku ya vazi la hijab hasa mashuleni.
Majaji hao pia walitoa wito kwa walimu kutofanya ubaguzi wa aina yoyote dhidi ya wanafunzi kwa misingi ya mavazi yao wala imani zao za kidini.
Kwa upande mwengine, Kadhi Mkuu wa Kenya Hammad Mohammed Kassim alitoa maelezo na kusisitiza kwamba vazi la hijabu ni mojawapo ya masharti kwa wanawake wa Kiislamu.
