Thursday, 15 September 2016

BALOZI WA UINGEREZA ASILIMU NA KUTEKELEZA IBADA YA HIJJA MWAKA HUU

Balozi wa Uingereza nchini Saudi Arabia, Simon Collis, ametekeleza ibada ya Hija mwaka huu baada ya kusilimu.

Collis ambaye aliteuliwa Januari 2015 kuwa balozi wa Uingereza nchini Saudia, aliikubali dini tukufu ya Kiislamu maishani hivi karibuni.
Collins na mkewe Huda
Katika picha zilizosambazwa katika mtandao wa twitter, Collis ameonekana akiwa ameandamana na mke wake, Huda Mujarkech, huku akiwa amevalia vazi maalumu la Hija la Ihram wakiwa katika eneo la Mina walipokuwa wakitekeleza amali za Hija.

Balozi Collis kupitia mtandao wa kijamii amemshukuru Fawziah Albakr ambaye ametuma picha hizo za awali katika mitandao ya kijamii. 

Katika maandishi yaliyoandamana na picha, Albakr aliandika, "Balozi wa kwanza wa Uingereza Saudia kutekeleza Hija baada ya kusilimu: Simon Collis na mke wake, Huda wakiwa Makkah."

Baada ya kujiunga na Wizara ya Mambo ya Nje ya Uingereza mwaka 1978, Collis aliwahi kuhudumukama balozi wa Uingereza Iraq, Syria, na Qatar mbali na kuwa afisa wa kidiplomasia Dubai, Basra, Tunis, New Delhi na Amman.