Mufti wa Tanzania, Sheikh Mkuu Abubakary Zubeir ameunda tume ya wajumbe wanane kwa ajili ya kushughulikia masuala mbalimbali, ikiwamo misamaha ya kodi iliyoombwa na Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) na taasisi zake.
Walioteuliwa kwenye tume hiyo ni Sheikh Abuubakar Khalid (mwenyekiti), Sheikh Issa Athman Issa (makamu) na Mwalimu Salim Ahmed Abeid ( katibu).
Wajumbe wengine ni Ustadh Tabu Kawambwa, Mwalimu Ally Abdallah Ally, Alhaj Omar Igge na Sheikh Omary Khamis.
Waraka uliosainiwa na Mufti Zubeir ulisema tume hiyo inapaswa kutoa mapendekezo kwake ndani ya siku 90 kuanzia tarehe ya kuanza kwake kazi.
Pamoja na mambo mengine, tume hiyo ina jukumu la kufuatilia mikataba yote ya uuzwaji wa viwanja na mali mbalimbali za baraza hilo na taasisi zake ili kuona uhalali wa umiliki huo.
Waraka huo unabainisha kuwa tume hiyo itahakikisha inafuatilia mikataba yote ambayo waliingia na wawekezaji ili kuona kama ina masilahi kwa Baraza na taasisi zake au la.
