Karibu mameya 30 wa Ufaransa wametakiwa kuzingatia uamuzi wa mahakama uliositisha amri ya tata ya kupiga marufuku uvaaji wa burkini kwenye miji ya mwambao.
Mahakama ya juu zaidi ya utawala nchini Ufaransa ilisitisha marufuku hiyo iliyowekwa mjini Villeneuve-Loubet siku ya Ijumaa kwa misingi ya haki za raia.
hata hivyo, mameya kadhaa wamesema wataendelea kutekeleza marufuku dhidi ya uvaaji wa Burkini.
Wakili wa masuala ya haki za binadamu aliyepinga marufuku hiyo mahakamani siku ya Ijumaa amesema kuwa atapeleka kila mji mahakamani.
Uamuzi wa mahakama ulibaini kuwa marufuku iliyowekwa katika mji wa Villeneuve-Loubet " ni ukiukaji mkubwa wa haki za kimsingi za uhuru".
Mamlaka za miji ya Nice na Frejus, pamoja na wale wa kijiji cha Sisco, wameapa kuendeleza marufuku hiyo kwenye maeneo yao.
Akijibu kuhusu uamuzi huo , meya wa Villeneuve-Loubet, Lionnel Luca, alisema : "Tunahitaji kuamua kama tunahitaji kutekeleza sharia ya kiislam kwenye maeneo ya fukwe au tunataka sheria za jamuhuri ya Ufaransa zitekelezwe."
Waziri mkuu wa Manual Valls aliandika kwenye ukurasa wake wa Facebook akiunga mkono marufuku zilizowekwa , akisema, burkinis ni "Kuidhinishwa kwa siasa ya Uislam katika maeneo ya umma".
Wakili wa baraza la miji , Francois Molinie, aliliambia gazeti la Ufaransa le Monde kwamba mameya wa miji wanaoendelea kutekeleza marufuku hiyo wanaweza kuiendeleza kwa muda mfupi.
Hata hivyo , alisema kwamba wanaweza kukabiliwa na hatua za kisheria katika mahakama ya utawala ambayo msingi wake unaweza kuwa ni uamuzi uliotolewa na mahakama ya juu zaidi.
Burkinis hazikutajwa kwa jina katika tangazo la marufuku, ambapo amri ilisema tu vazi la mwambao ama ufukweni linapaswa kuwa la kushima kwa umma na misingi ya kutoashiria dini yoyote.
Mamlaka zilisema kwamba zilikuwa na hofu juu ya usalama wa jamii kuhusiana na nguo za kidini, hususan baada ya mashambulio katika miji ya Nice na Paris yaliyochochewa na waislamu wenye itikadi kali.

