Tuesday, 14 June 2016

MAUAJI YA ORLANDO, TRUMP ACHOCHEA ZAIDI CHUKI DHIDI YA WAISLAMU MAREKANI

Mgombea wa kiti cha urais wa chama cha Republican nchini Marekani Donald Trump, amesema mauaji ya watu 50 katika baa moja ya wapenzi wa jinsia moja huko Orlando inathibitisha msimamo wake kwamba waislamu wapigwe marufuku kukanyaga ardhi ya Marekani.

Trump amemkashifu mpinzani wake wa chama cha republican Bi Hillary Clinton, kwa kutodadisi sababu za mtu huyo kutenda mauaji hayo.
Wakati huo huo Shirika la kijasusi la FBI limesema mtu aliyewaua watu 50 kwa kuwafyatulia risasi katika klabu moja ya wapenzi ya jinsia alikiri kuunga mkono kundi la kigaidi la IS.

Fbi wameongeza kusema kuwa wamekuwa wakimfanyia uchunguzi mtu huyo Omar Seddique Mateen tangu 2013 baada ya kutoa matamshi ya chuki akiwa kazini.

Babake Mateen amesema anaamini kitendo alichokifanya mwanawe kilitokana na msukumo wa hisia zake dhidi ya wanaondeleza mapenzi ya jinsia moja na wala si kwa sababu za kidini.

Naye mkewe wa zamani Sitora Yusufiy, amemwelezea Mateen kama mtu wa aliyekuwa tabia za kigomvi na kutaka kupiga watu lakini hakuwa na itikadi kali za kidini.

Kufuatia hali hiyo, Baraza la Mahusiano ya Kiislamu Marekani (CAIR) limelaani hujuma katika mji wa Orlando nchini Marekani ambapo watu wasiopungua 50 waliuawa katika klabu moja huku wengine 53 wakijeruhiwa.

Aliyetekeleza mauaji hayo anadaiwa kuwa muungaji mkono wa kundi la kigaidi la ISIS au Daesh.

Kundi la kigaidi la ISIS limetangaza kuhusika na hujuma hiyo. Katika taarifa, CAIR imetaja mauaji hayo kuwa ni jinai ya chuki ambayo inalaaniwa vikali. 

Mwenyekiti wa Baraza la Mahusiano ya Kiislamu Marekani Nihad Awad amesema mauaji hayo yanakiuka misingi ya Marekani na Waislamu. Aidha amesisitiza kuwa ISIS ni kundi haramu lisilowakilisha Waislamu.