Tuesday, 15 December 2015

WASIWASI WA USALAMA KATIKA MISIKITI YA MAREKANI WAONGEZEKA

Viongozi wa kiislamu wa misikiti iliyopo vitongoji vya Los Angeles hadi nje ya mji Washington DC wameonyesha kuongezeka kwa hofu kuhusu usalama wa waislamu kufuatia kuwa na chuki kutoka kwa umma baada ya mashambulizi mjini Paris na San Bernardino.

Wito wa mgombea wa urais wa chama cha Republican Donald Trump wa kutaka waislamu kupigwa marufuku kuingia Marekani umezua hofu zaidi katika jamii ya waislamu Marekani.

Misikiti kadhaa nchini Marekani imewekwa chini ya ulinzi kutoka idara ya nchi ya usalama.
Mwishoni mwa wiki polisi walimtia  mbaroni kijana wa kiume mwenye umri wa miaka 23 baada ya kutuhumiwa kujaribu kuchoma moto msikiti mmoja katika jimbo la California.

Shambulizi lilokuwa lifanyike California linakisiwa la kulipiza kisasi baada ya waislamu kushutumiwa kuhusika na shambulizi la San Bernardino lilotokea tarehe 2 Desemba.

Siku ya Ijumaa moto uliwekwa katika lango la jumba la chama cha kiislamu cha Coachella na kusababisha majeraha kwa watu kadhaa.

Kufuatia kuongeza  kwa uhasama imekuwa ngumu kwa viongozi wa kiislamu kuajiri walinzi kwani walinzi wengi pia wanahofia maisha yao.

Walinzi wengi katika maeneo ya Dulles vitongoji vya Washington na Virginia ambavyo vina idadi kubwa zaidi ya waislamu wamejiondoa kazini baada ya mashambulizi ya San Bernardino.