Saturday, 12 December 2015

MWANAWE MUAMMAR GADDAFI AACHILIWA HURU

Hannibal Gaddafi ambaye ni mwana wa kiongozi wa zamani wa Libya Muammar Gaddafi, ameripotiwa kuachiliwa huru na kuwasilishwa kwa vikosi vya usalama vya Lebanon.

Kulingana na taarifa za kituo kimoja cha televisheni, Hannibal Gaddafi alikuwa ametekwa nyara na kundi moja lililojihami katika eneo la Bekaa.
Kituo hicho cha televisheni kilichapisha kanda ya video iliyomuonesha Hannibal Gaddafi akisema kwamba yupo katika hali nzuri na alikuwa ametekwa nyara na kundi la watu 'wanaodai ukweli na haki'.

Hannibal Gaddafi pia alisema kwamba kundi hilo la watekaji nyara kuwa ni la wafuasi wa Imam Moussa al-Sadr ambaye ni kiongozi wa Shiite na mwanzilishi wa chama cha harakati cha AMAL, aliyewahi kupotea mwaka 1978 wakati wa ziara ya Libya.

Hannibal Gaddafi, mkewe, mwanawe wa kiume Mohammed pamoja na mwanawe wa kike Aisha, ni baadhi ya watu waliokimbilia nchini Algeria baada ya Muammar Gaddafi kupinduliwa nchini Libya.