Wednesday, 12 March 2014

MUSWADA WA KUPIGA MARUFUKU SKETI FUPI, KUSHUSHA SURUALI KATIKA MAKALIO WAPELEKWA BUNGENI KENYA

Kaunti ya Kilifi huenda ikawa ya kwanza nchini Kenya kuzima uvaaji wa sketi fupi (mini Skirt) katika maeneo yurualia umma, ikiwa mswada ulioletwa na mwakilishi wa wadi ya Marafa Renson Karisa Kambi utapitishwa na kuwa sheria.

Mswada huo unapanga kuzima kabisa uvaaji wa sketi fupi katika maeneo ya umma na vile vile kuvaa nguo za kuonyesha ndani kama zile za kulalia hadharani.

Mswada huo vile vile utaangalia uwezekano wa kuzima uvaaji wa sketi fupi katika wasichana wa shule na vile vile uvaaji wa long’i ambazo zinawaonyesha wavulana makalio yao pamoja na uvaaji mbaya wa makanga katika matatu.

Akiongea na Taifa Leo kwa njia ya simu, naibu spika wa bunge la kaunti ya Kilifi, Bw Teddy Mwambire, alisema kuwa mswada huo unalenga kuhifadhi mila za mpwani ikiwemo uvaaji nadhifu ambao jamii hiyo imelinda kwa miaka na vikaka.

Aidha Bw Mwambire alisema kuwa licha ya juhudi za kujaribu kuhifadhi mavazi ya kitamaduni lakini pia kumekuwa na chimbuko baya la wasichana na wavulana kuvaa nusu uchi hasa katika miji inayopanuka kwa haraka kama vile Mtwapa, Watamu na Malindi.

“Tunahusika kama viongozi kuona kwamba watoto wetu wanavaa nguo za heshima na zenye hadhi. Hatuwezi kutekwa na mila ambazo hazina msingi wowote na jambo hili linaweza kuwa tatizo kubwa kwetu,” alisema.

Naibu huyo wa spika alisema kuwa vijana wengi wamechanganyikiwa kwa kuiga tamaduni za kimagharibi, ikiwemo uvaaji duni ambao umewafanya wengi wao kukosa kujua mavazi  bora ya kuvaa.

Akiongea kwa njia ya simu, mjumbe wa wadi ya Marafa ambaye ndiye muasisi wa mswada huo Bw Renson Kambi alisema kuwa aliamua kujiri na mswada huo baada ya kuona hatari inayokodolea macho vijana wetu, hasa katika uvaaji.

“Ni jambo la kusikitisha kwamba hata katika shule zetu, mabinti wetu wamejiri na mfumo wa kuvaa sketi fupi fupi sana kiasi kwamba hata akiangusha kalamu hawezi kamwe kuiokota. Wanavaa zile sketi ambazo wanaita micro mini ambazo ni ndogo sana na hata wanapokuwa darasani wanakosa utulivu. Ninaamini kwamba wenzangu wakiniunga mkono kwa hoja hii, mambo yatabadilika,” alisema.

Alisema ingawa mswada huo bado uko katika sehemu za awali anaamini kuwa utakuwa na sheria ambayo itawatoza watakaoenda kinyume na uvaaji huo unaolengwa na sheria hiyo.

Maoni yake yaliungwa mkono na waziri wa masuala ya elimu na utamaduni katika kaunti ya Kilifi Salma Muhiddin ambaye alisema ni jambo la mwafaka kwani vijana wengi hata katika mashule ni waathirika wakuu katika uvaaji duni.

“Tuko katika shida kwani watoto wetu wamepoteza mwelekeo kwa kutojua ni nguo ipi nzuri ya kuvaa na ile ambayo hawafai kuvaa. Wengine hata utashangaa wanatembea nusu uchi na hii ni kunyume na tamaduni za watu wapwani hasa katika hali ya uvaaji,” alisema.