Tuesday, 4 March 2014

MAURITANIA WAANDAMANA KULAANI KUDHALILISHWA QURANI, MMOJA AFARIKI

Wananchi wa Mauritania jana wameandamana katika maeneo mbalimbali ya mji mkuu, Nouakchott kulaani kitendo cha kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu na kusababisha kifo kwa mtu mmoja. 

Katika maandamano hayo imeelezwa kijana mwenye umri wa miaka 21 alikufa kufuatia kuathiriwa na gesi zilizotokana na mabomu ya machozi yaliokuwa yakirushwa na polisi waliokuwa wanazuia maandamano hayo.

Maandamano hayo yenye hamasa yalifanyika kwa ajili ya kulalamikia hatua ya watu kadhaa kuvunjia heshima Qur'ani Tukufu katika msikiti mmoja mjini humo. Maandamano hayo yalikwamisha shughuli mbalimbali katika mji mkuu.

Imamu wa msikiti huo Mohamedoun Ould Mohamed SalemI anaeleza kuwa, watu wanne wasiojulikana usiku wa juzi waliingia katika msikiti mmoja kaskazini mwa mji wa Nouakchott na kuchana nakala za Qur'ani katika msikiti huo na kuzitupa katika choo cha msikiti. 


Polisi imeanza uchunguzi kubaini watu waliohusika na tukio hilo la udhalilishaji wa Qurani tukufu. Mauritania ina watu karibu milioni 3 na nusu na karibu wote ni Waislamu.