Friday, 28 February 2014

WANAFUNZI WATOROKA SHULENI KUHOFIA MASHAMBULIZI YA BOKO HARAM

WANAFUNZI wa shule za bweni kaskazini mwa Nigeria wametoroka shule hizo baada ya shambulizi lililotekelezwa na  wanamgambo  wa Boko Haram katika shule moja ambapo wanafunzi 43 waliuawa kwa kupigwa risasi na kukatwa kwa upanga huku shule hiyo ikiteketezwa.

Wanafunzi  hao waligomba kulala shuleni na vyuoni mwao baada ya tukio hilo katika shule ya Federal Government iliyoko mjini Buni Yadi, katika jimbo la Yobe Jumanne.

“Wanafunzi wengi katika shule za mabweni wameondoka na kwenda makwao baada ya  kupashwa habari kuhusu shambulizi  la Buni Yadi,” Yunusa Ahmed anayeishi katika mji mkuu wa Damaturu aliambia AFP.

Mwanawe  wa kiume Ahmed  ni mwanafunzi katika Government Secondary School na amerejea nyumbani kwao pamoja na wenzake. “Walienda shuleni Jumatano lakini wamerudi nyumbani kwani hawataki kulala shuleni humo kutokana na hofu ya kushambuliwa na Boko Haram,” Ahmed alisema.

Kundi la Boko Haram linapinga masomo ya kigeni na imeteketeza mamia ya shule katika mapigano yake ya miaka minne na nusu yanayolenga kubuni jimbo la kiislamu kaskazini mwa Nigeria. Jina “Boko Haram” kwa Kihausa lamaanisha “Elimu ya Kigeni ni dhambi”.

Mwezi Oktoba mwaka jana maafisa wa Serikali katika jimbo la Yobe walisema wapiganaji wa kundi hilo waliteketeza shule 209, na kusababisha hasara ya kiasi cha dola 15.6 milioni za Marekani.

Mashambulizi hayo yanaathiri sekta ya elimu katika eneo hilo ambalo tayari liko nyuma katika nyanja za maendeleo  likilinganishwa na maeneo mengine nchini Nigeria.

Akihutubia taifa kupitia runinga  Jumatano jioni, Rais Goodluck Jonathan alisema wanafunzi hao waliuawa kikatili.

Boko Haram