Waziri Mkuu Abdiweli Sheikh Ahmed aliwahutubia wananchi katika maandamano hayo yaliyotayarishwa na Wizara ya Wanawake na Haki za Binadamu ya Somalia, serikali ya mkoa wa Benadir na asasi za kiraia, ambapo alitoa wito kwa Wasomali kusimama dhidi ya Al-Shabaab.
"Wanawake wa Kisomali leo wamekusanyika hapa kuthibitisha utayari wao wa kushiriki kwenye kampeni ya kitaifa ya kuikomboa nchi hii kutoka kwa wenye siasa kali ambao hawasimamii chochote zaidi ya mauaji ya Wasomali wasio na hatia," alisema Waziri wa Wanawake na Haki za Binadamu, Khadijo Mohamed Diriye.
Baada ya maandamano hayo, Ahmed aliongoza kikao cha dharura cha baraza lake la mawaziri, meya wa Mogadishu, wakuu wa wilaya za Benadir na vyombo vya usalama juu ya hatua za ulinzi mjini Mogadishu.
"Wale walioishambulia kasri yetu ya rais ni maadui wa nchi yetu, hatutawaruhusu kujificha na kutushambulia tena", alisema kwenye taarifa yake.
Aliongeza kusema kuwa, "Serikali hii pamoja na watu wa Somalia na jumuiya ya kimataifa tutafanya kazi pamoja kupambana na magaidi hawa, kuhakikisha usalama wa mitaa yetu na kuiendeleza nchi yetu."
Serikali hiyo ilitangaza kuundwa kwa kamati ya kuchunguza vipi mashambulizi hayo yalitokea, nani alishiriki na kwa nini hayakuzuiwa. Ripoti inatarajiwa mwishoni mwa wiki hii.
Maandamano hayo yalifanyika siku mbili baada ya Al-Shabaab kufanya mashambulizi mabaya kabisa ya kujitioa muhanga kwenye jengo la Villa Somalia, na kuwaua kiasi cha maafisa na wanajeshi watano wa Somalia.
Hata hivyo, kiongozi wa Al-Shabaab katika mkoa wa Benadir, Sheikh Ali Mohamed Hussein, aliripoti idadi kubwa zaidi ya waliouawa.
Alisema waliuwa raia 16 wa Uganda, walinzi 17 wa rais na maafisa 12 wa usalama ambao waliwasili hapo kama kikosi cha kuongeza nguvu, kwa mujibu wa mtandao unaoiunga mkono Al-Shabaab, Somali Memo.
Pia katika siku hiyo ya Jumapili, maafisa wa usalama wa Somalia na wa Misheni ya Umoja wa Afrika nchini Somalia walifanya msako wa nyumba hadi nyumba katika wilaya za Mogadishu, na kuwakamata washukiwa kadhaa, uliripoti mtandao wa Hiraan Online wa Somalia.
![]() |
| wanawake wa kisomali wakiandamana |
