Monday, 24 February 2014

RAIS MUSEVENI AMWAMBIA OBAMA ASIINGILIE MASUALA YA NDANI YA UGANDA

Rais Yoweri Museveni wa Uganda ametoa matamshi makali dhidi ya Rais Barack Obama wa Marekani akimtaka akome kuingilia masuala ya ndani ya Uganda.

Matamshi hayo makali yamekuja baada ya Rais wa Marekani kutishia kuwa uhusiano wa nchi yake na Uganda utaharibika iwapo Rais Museveni atasaini na kuufanya kuwa sheria muswada wa kupinga vitendo vichafu vya kujamiiana watu wa jinsia moja.

Rais Museveni amesema, atashirikiana na Russia iwapo Marekani itaendelea kuingilia masuala ya ndani ya Uganda na kuongeza kuwa, "Russia imekuwa ikifanya shughuli zake barani Afrika tangu mwaka 1917 yaani kwa zaidi ya miaka 100. Ninataka kushirikiana na Russia kwa sababu hawachanganyi siasa zao na siasa za nchi nyingine." 

Ameongeza kuwa, "Ukiona mtu anaingia ndani ya nyumba ya mtu mwingine basi jua kuna tatizo. Hapa ni nyumbani petu. Huwezi kumuona mtu mwenye upaa kama mimi hivi ndani ya nyumba yake na kuanza kumpangia afanye unavyotaka wewe. Rudi kwenu!".


Rais Museveni ameahidi kusaini muswa unaotaka watu wanaojihusisha na ushoga kufungwa maisha Jela. 

Muswada huo ulipitishwa na wabunge wa Uganda mnamo Desemba mwaka jana baada ya wale walioinakili kuondoa sehemu iliyopendekeza hukumu ya kifo. 

Chini ya sheria hiyo iliyopendekezwa, watu watakaopatikana na hatia ya kujihusisha na vitendo vya ushoga watakabiliwa na hukumu kali, ikiwemo kifungo cha maisha jela.

Hatua hiyo ambayo imeibua malalamishi makali kimataifa, itaharamisha utangazaji au utambuzi wa uhusiano wa kimapenzi kati ya watu wa jinsia moja.
Obama alisema kuwa rais wa Uganda, ambaye ni kiongozi muhimu kutoka Afrika kwa utawala wa Marekani na Muungano wa Ulaya, huenda akapelekea kuwepo kwa uhusiano mbaya kati ya nchi yake na Marekani ikiwa ataidhinisha mswada huo kuwa sheria.

Februari 6 mwaka huu Museveni, ametia saini sheria mpya inayotoa adhabu kali kwa wanaopatikana na hatia ya kutembea nusu uchi au kuhusika na vitendo vinavyohusisha picha za ngono.
Yoweri Museveni