Monday, 24 February 2014

BAN KI-MOON AWASIHI WANANCHI WA JAMHURI YA AFRIKA YA KATI KUWEKA SILAHA CHINI

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon amewata wale wote wenye silaha nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati waweke chini na kurudisha amani ya nchi hiyo.

Ban Ki-Moon amezungumza na wananchi wa Jamhuri ya Afrika ya kati kwa lugha ya Sango ya huko Jamhuri ya Afrika ya Kati, kupitia njia ya radio.

Baada ya salamu Bwana Ban ambaye ametuma ujumbe huo pia kwa lugha ya Kifaransa na kiingereza, amewahakikishia wananchi hao walio katika zahma ya mapigano ya kwamba hawako peke yao.

Aidha, Katibu Mkuu amesema yuko pamoja na wananchi hao na amewaahidi usaidizi wake wote kwa ajili ya amani na maridhiano, haki na uwajibikaji kwa wananchi wote wa Jamhuri ya Afrika ya Kati. 

Ujumbe kamili wa Ban Ki-Moon:-
"Niko hapa kueleza mshikamano wangu na usaidizi kwa wananchi wa Jamhuri ya Afrika ya Kati. Hamko peke yenu! Mataifa mengi yanajitahidi kusaka amani! 

Nimeomba jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua zaidi! Askari na polisi wengi wanalinda raia, misaada zaidi kuokoa maisha. Nawasihi na ninyi, wananchi wa Jamhuri ya Afrika ya Kati na upinzani, acheni mauaji. 

Acheni mauaji. Wekeni silaha zenu chini. Wale wanaofanya ghasia wanaigawa na kuiharibu nchi yenu pendwa. Waislamu na wakristu mmejenga nchi yenu kwa pamoja. Nafahamu mtafanya hivyo tena."


Ban Ki-Moon