Thursday, 27 February 2014

KWA KUPITISHA SHERIA DHIDI YA MASHOGA, MBUNGE WA MAREKANI APENDEKEZA UGANDA INYIMWE MISAADA

MBUNGE mmoja mwenye ushawishi mkubwa Jumanne alipendekeza kusitishwa kwa msaada unaopelekwa Uganda baada ya rais wa nchi hiyo kutia sahihi sheria mpya itakayowafanya mashoga na wasagaji wahukumiwe vifungo vya maisha.

“Uamuzi wa Rais (Yoweri) Museveni wa Uganda wa kutia sahihi sheria ya mashoga na wasagaji umenitia hofu,” Seneta Patrick Leahy, ambaye ndiye seneta mkongwe zaidi katika bunge hilo na anayeongoza Kamati ya Haki, alisema kupitia taarifa.

“Msaada mwingi wa Amerika kwa Uganda unawalenga watu wa Uganda, wakiwemo wale wa jamii ya LGBT (wasagaji, mashoga, wenye jinsia mbili na wanaogeuza jinsia zao) ambao haki zao za kibinadamu zimekiukwa,” akaongeza.

“Lakini tunapaswa kutathmini upya msaada wote wa Amerika kwa  Uganda, ikiwemo kupitia Benki ya Dunia na mashirika mengine.”

Amerika ni miongoni mwa wafadhili wakubwa wa kimataifa wa Uganda. Serikali hiyo ilisema kwamba mwaka huu wa kifedha, dola 485 milioni zimepelekwa Uganda huku kiwango kikubwa cha pesa hizo kikipelekwa kwa miradi ya kiafya, elimu, lishe na mafunzo ya kijeshi.


Seneta Patrick Leahy