Sunday, 13 August 2017

WATU MILIONI 2 WATEMBELEA JUMBA LA MAKUMBUSHO LA QURANI MADINA

Mkurugenzi wa Jumba la Makumbusho la Qur’ani Tukufu katika mji wa Madina nchini Saudi Arabia, Hamza Musa Adam amesema jumba hilo limetembelewa na wageni milioni mbili katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo katika jumba hilo kuna nakala nyingi zilizoandikwa kwa mkono na pia nakala 57 nadra za Qur’ani Tukufu.

Amesema nakala ya kale zaidi ni iliyoandikwa mwaka 488 Hijria Qamaria (1095 Miladia). 

Aidha ameongeza kuwa moja ya nadra za Qur’ani katika maonesho hayo ni ile yenye uzito wa kilo 154 iliyoandikwa karne mbili zilizopita.

Adam amesema wageni katika Jumba la Makumbusho la Qur’ani Tukufu mjini Madina wanapokea maelezo kwa lugha 13. 

Amesema tokea kuanzishwa kwake mwaka 2015, jumba hilo la makumbusho limepokea wageni milioni mbili kutoka maeneo mbali mbali duniani huku idadi ya wanaofika hapo ikitazamiwa kuongezeka katika msimu wa Hija mwaka huu.