Sunday, 27 August 2017

CHUO KIKUU CHA QURAN KUANZISHWA MALAYSIA

Chuo Kikuu cha Qur’ani kinatazamiwa kuanzishwa nchini Malaysia katika jimbo la Baling baada ya mbunge wa eneo hilo kuahidi kutenga ardhi ya hekari 12.8 kwa ajili ya mradi huo.

Mbunge Abdul Aziz Abdulrahim amesema ardhi itatolewa wakfu kisha ikabidhiwe kwa Jumuiya ya Kitaifa ya Kuhifadhi Qur’ani Malaysia, kwa ajili ya ujenzi wa chuo hicho. Amesema serikali ya Malaysia pia itashiriki katika ujenzi wa chuo hicho.

"Nitatafuta ardhi ya wakfu katika eneo la Baling na kisha nitaikabidhi kwa Jumuiya ya Kitaifa ya Kuhifadhi Qur’ani Malaysia (Permata al-Quran) na baada ya hapo nitafanya mazungumzo na Waziri Mkuu Datuk Seri Najib Razak kuhusu ujenzi wa chuo hicho,” alisema mbunge huyo.

Nchini Malaysia kuna vyuo 519 vikubwa vya kuhifadhi Qur’ani ambavyo vimesajiliwa rasmi huku kukiwa na vingine vingi ambavyo havijasajiliwa.

Malaysia ni nchi ya Kiislamu ya Asia ya kusini-mashariki kando ya Bahari ya Kusini ya China na dini rasmi nchini humo ni Uislamu ambapo karibu asilimia 65 ya wakaazi wote milioni 32 nchini humo ni Waislamu.