Friday, 14 March 2014

VIONGOZI WA DINI JAMHURI YA AFRIKA YA KATI WAOMBA UMOJA WA MATAIFA KUHARAKISHA JESHI LA ULINZI WA AMANI NCHINI HUMO

Viongozi wa madhehebu ya kiislamu na kikristo kutoka Jamhuri ya Afrika ya Kati wamesihi Umoja wa Mataifa kuchagiza mpango wa kupeleka ujumbe wake wa kulinda amani nchini humo ili kuepusha kuendelea kuzorota kwa amani nchini humo.

Wamesema hayo katika kauli zao mbele ya waandishi wa habari mjini New York baada ya mazungumzo na Katibu Mkuu Ban Ki-Moon ambaye naye kwenye mkutano huo amesema ushirikiano wa viongozi hao ni ishara thabiti ya utamaduni wa siku nyingi wa kuishi pamoja nchini humo.

Viongozi hao ni pamoja na Askofu Mkuu wa jimbo katoliki Bangui na mkuu wa kanisa katoliki nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati Monsignor Dieudonné ambaye ametoa shukrani.

“Twapenda kushukuru mataifa yote yaliyokubali kuchangia kwa maslahi ya wananchi wa Jamhuri ya Afrika ya Kati waliojificha vichakani. Tunauomba Umoja wa Mataifa kuchukua hatua haraka kuokoa maisha ya raia hao."

Kiongozi wa Kiislamu, Imam Omar Kobine Layama naye alisisitiza kuwa, “Tunaamini Katibu Mkuu kuwa gharama ya ujumbe wa ulinzi wa amani ni kubwa sana, lakini kwa kufikiria ugumu wa janga husika, kupelekwa kwa operesheni ya ulinzi wa amanini jambo la dharura sana."

Naye katibu Mkuu wa umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon alisema, “Mzozo wa Jamhuri ya Afrika ya Kati si wa kidini. Ukweli ni kwamba udini na ukabila umetumika tu kwa maslahi ya kisiasa. Viongozi wa kidini walioko hapa wanakataa fikra ya kwamba wao ni maadui. Hawavumilii mgao baina ya makundi mbali mbali kwenye jamii. Ni wajibu wa jamii ya kimataifa kuwapatia ushirikiano thabiti."

Mapigano nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati yalianza Disemba 2012 na kwa mujibu wa viongozi hao wa kidini wakati umefika vikundi vyenye silaha vipokonywe na serikali ya mpito ipatiwe uwezo wa kuendesha nchi.

Katibu Mkuu Ban Ki-Moon akiwa na viongozi wa kidini kutoka CAR.
Kutoka kushoto Imam Omar Kobine Layama, Mchungaji Nicolas Guérékoyamé Gbangou na
Askofu Mkuu Dieudonné Nzapalainga, baada ya mazungumzo mjini New York, Alhamisi.