Sunday, 2 February 2014

LIBYA MABINGWA WAPYA CHAN 2014, YAICHAPA GHANA 4-3

TIMU ya taifa ya Libya imetwaa ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN) 2014  baada ya kuifunga Ghana kwa penalti 4-3 kufuatia sare ya bila kufungana Jumamosi Uwanja wa Cape Town. 

Ushindi huo ni sawa na Libya kulipa kisasi kwa Ghana baada ya kufungwa kwa penalti 7-6 miaka 32 iliyopita kwenye fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON).

Kipa wa Ghana, Stephen Adams aliokoa penalti mbili za Mohamed Elgadi na Abdelsalam Omar na kufanya mikwaju mitano mitano ya awali imalizike kwa sare ya 3-3.

Ahmed El Trbi aliifungia penalti ya sita Libya kabla ya Joshua Tijani kukosa upande wa Ghana na kuamsha shamrashamra za wafalme wa Mediterranean Knights wa Libya. 

Katika mchezo uliotangulia kusaka mshindi wa tatu, Nigeria iliifunga Zimbabwe 1-0 na kushinda Medali ya Shaba ya michuano hiyo ya tatu. 

Libya inakuwa bingwa wa tatu tangu kuanzishwa CHAN, michuano inayohusisha wachezaji wanaocheza ligi za nchini mwao pekee, wakifuata nyayo za DRC 2009 nchini Ivory Coast na Tunisia 2011 nchini Sudan.


Wakishangilia kwa namna ya kusujudu