Watu wanaodaiwa kuwa wapiganaji wa kundi la Boko Haram la nchini Nigeria wamewaua zaidi ya watu 90, wakiwemo watoto na wanawake, katika shambulizi kwenye kijiji kimoja kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.
Kwa mujibu wa mashuhuda, shambulizi hilo limetokea katika kijiji cha Izghe katika jimbo la Borno jana.
Mashuhuda hao wanasema kuwa wanamgambo wenye silaha na mabomu, walikizunguka kijiji hicho na kukishambulia kwa risasi. Aidha, inadaiwa kuwa walizichoma moto nyumba kadhaa.
“Wakati huu ninapozungumza na wewe, maiti za watu waliouawa bado zimelala mitaani,” mkazi wa kijiji hicho, Abubakar Usman alisema na kuongeza, “tulikimbia kuwazika, kwa hofu kwamba wauaji bado wanasubiri porini.”
Kamishna wa polisi katika jimbo la Borno, Lawal Tanko, amethibitisha kutokea kwa shambulizi hilo lakini akasema kuwa maelezo ya kina juu ya shambulizi hayo hayajathibitishwa.
Shambulizi hilo ni jipya kabisa katika mfululizo wa wimbi la ghasia katika eneo hilo la kaskazini mashariki mwa Nigeria.
Mnamo Mei 2013, Rais wa Nigeria, Goodluck Jonathan, alitangaza hali ya hatari katika majimbo matatu kaskazini mashariki mwa nchi hiyo, ambayo ni Borno, Yobe, na Adamawa.
Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonesha kuwa
zaidi ya watu 1,200 wamepoteza maisha katika ghasia nchini humo tangu hali hiyo ya hatari ilipotangazwa.
Kundi la Boko Haram (Taaluma kutoka Magharibi ni Haramu) linasema kuwa lengo lake ni kuiondosha serikali ya Nigeria.
Kundi hilo linadai kuhusika na mashambulizi kadhaa katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo tangu mwaka 2009.
