Sunday, 16 February 2014

ANT-BALAKA WAANZA KUPORWA SILAHA JAMHURI YA AFRIKA YA KATI

Vikosi vya Umoja wa Afrika vilivyoko katika Jamhuri ya Afrika ya Kati vimeanza operesheni ya kuwapokonya silaha wanamgambo wa Kikristo wa Anti-Balaka katika mji mkuu Bangui. 

Gazeti la Kifaransa la Le Figaro toleo la mtanadao linaripoti kwamba, vikosi vya Umoja wa Afrika vikishirikiana na majeshi ya Ufaransa asubuhi ya jana vilianza operesheni ya kuwapokonya silaha wanamgambo wa Kikristo wa Anti-Balaka wanaowauwa Waislamu. 

Taarifa zaidi zinasema kuwa, operesheni hiyo ya upokonyaji silaha imeanza katika eneo linalojulikana kwa jina la Boy-Rabe mjini Bangui. 

Operesheni hiyo ya upokonyaji silaha ya nyumba hadi nyumba imepelekea kupatikana silaha nyingi. 

Wakati huo huo, Francois Bozize, Rais wa zamani wa Jamhuri ya Afrika ya Kati ameikosoa serikali ya sasa ya nchi hiyo akisema kwamba, imeshindwa kuendesha nchi. 

Bozize amesema kwamba, hakuna wakati ambao nchi hiyo ilikabiliwa na hali mbaya ya ukosefu wa amani kama ilivyo hivi sasa. 

Kiongozi huyo wa zamani wa Jamhuri ya Afrika ya Kati aliyeondolewa madarakani na waasi wa zamani wa Seleka amesema kuwa, demokrasia imekuwa muhanga wa hali inayotawala hivi sasa nchini humo na kwamba, serikali ya muda ya nchi hiyo imeitumbukiza nchi katika dimbwi la damu na mauaji makubwa.


Wakivunja Msikiti