Friday, 21 July 2017

ZAKIR NAIK APOKONYWA PASIPOTI NA SERIKALI YA INDIA

Mhubiri maarufu Zakir Naik amepokonywa pasi yake ya kusafiria na serikali ya India.
Taarifa zinasema serikali ya India imechukua uamuzi huo Jumanne baada ya serikali ya India kusema anatakiwa kujibu mashtaka kuhusu tuhuma za kufadhili ugaidi. 

Pasi ya kusafiria ya Naik, raia wa India, imechukuliwa na serikali ya nchi hiyo kufuatia ombi la Shirika la Kitaifa la Upelelezi (NIA)

Maafisa wa shirika hilo kuu la upelelezi India wanasema pasipoti hiyo imebatilishwa na Idara ya Kieneo ya Pasipoti ya Mumbai baada ya Naik kukataa kutii agizo la kufika katika idara za upelelezi kama alivyotakiwa kufanya mnamo Julai 13.

Naik alikuwa ametakiwa kufika katika idara hiyo ajitetee na aeleze kwa nini pasi yake haipaswi kubatilishwa kwa kuzingatia kesi kadhaa dhidi yake.

Alitoroka India Julai 1, 2016 baada ya magaidi katika nchi jirani ya Bangladesh kudai kuwa walivutiwa na hotuba zake na wakaamua kutekeleza hujuma zao za kigaidi.

Vyombo vya habari India vinasema Naik tayari ameshapata uraia wa Saudi Arabia lakini hakuna chombo rasmi kilichothibitisha taarifa hiyo hadi sasa. 

Tayari serikali ya India imeshapiga marufuku Taasisi ya Utafiti wa Kiislamu (IRF) inayosimamiwa na Dkt. Naik. 

Mhubiri huyo anamiliki pia televisheni iitwayo 'Peace TV'.